SIKU moja baada ya mahakama kuu ya Tanzania, kutoa hukumu ya kuusafisha uenyekiti wa Prof. Ibrahim Lipumba katika chama cha CUF, mwenyekiti huyo amewataka wanachama wa chama hicho hasa Zanzibar kuacha jazba.
Chini ya jaji Benhajj Masoud, mahakama hiyo juzi ilitoa uamuzi wa kukubali kwamba msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania alikuwa na haki ya kuendelea kuutambua uenyekiti wa Prof. Lipumba katika chama hicho.
Uamuzi huo ulitokana na baadhi ya viongozi wa chama hicho ukiongozwa na aliyekuwa katibu mkuu maalim, Seif Sharif Hamad, kufungua kesi nambari 23 ya mwaka 2016, kupinga msajili kuingilia maamuzi ya ndani ya chama pale alipotangaza kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti hasa ikizingatiwa kuwa alijiuzulu.
Muda mchache baada ya hukumu hiyo maalim Seif na viongozi wengine waliokuwa wa CUF walitangaza kuondoka katika chama hicho na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo, hatua ambayo imezidisha mpasuko mkubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba aliwataka wanachama wa CUF, hasa upande wa Zanzibar kumuunga mkono ili wajenge chama bila ya maalim seif na kuacha jazba.
Lipumba aliwasihi wafuasi wa CUF kuwa wakumbuke wametoka mbali na kwamba kuondoka mtu mmoja isiwe sababu ya kuvurugika kwa chama hicho.
“Chama hiki ni kimoja na tuna chama kimoja, hivyo tuendelea kuunga mkono chama chetu, sisi tulikuwa kipaumbele katika kudai haki ya kupata katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, utawala bora”, alisema Prof. Lipumba
Prof.Lipumba alibainisha kuwa hakuna mtu aliyetetea haki za wazanzibari kama yeye, hivyo basi historia inaonesha hakuna kama yeye na kuwataka Seif Sharif asiwafarakanishe.
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema wazanzibari wanapaswa kutambua kuwa maalim Seif ni mtu hatari kwani ametawaliwa na ubinafsi huku akimshangaa kuhama chama kwenda ACT na kuwataka wabunge wamfuate.
“Kwa sasa nina kazi ya kuponya majeraha yaliyotokana na mgogoro wa kiuongozi wa CUF, wanachama wa chama hicho hasusani wa wazanzibari wasiingie jazba kuchoma bendera zozote ni kosa la jinai kubadilisha ofisi ya chama, ofisi ya Mtendeni ni ya chama”, alisema Prof. Lipumba.
HAFSA GOLO NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM